Eddy Kenzo asifia simulizi za Bobi Wine katika nyimbo

Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alisema akichipuka, alipenda kusikiliza muziki wa Bobi Wine.

Marion Bosire
1 Min Read
Eddy Kenzo

Msanii wa Uganda Eddy Kenzo amemsifu Bobi Wine kwa uwezo wake wa kusimulia hadithi kupitia muziki, akisema nyimbo zake zimekuwa zikimvutia kwa namna ya kipekee.

Katika mjadala kuhusu wasanii watatu wakubwa nchini Uganda, maarufu kama ‘Big 3’, uwezo wa Bobi Wine wa kusimulia hadithi kupitia muziki umekuwa ukitajwa na wachambuzi kadhaa wa muziki. Kenzo pia anakubaliana na mtazamo huo.

Akizungumza katika mahojiano, Kenzo alisema alipokuwa msanii chipukizi alipenda kusikiliza muziki wa Bobi Wine kutokana na namna alivyokuwa akiwasilisha hadithi zake kupitia nyimbo.

“Nilivutiwa sana Bobi Wine, na nilipokuwa nikifanya maonyesho wakati wa siku zangu za karaoke, mara nyingi nilikuwa nikiimba wimbo wake ‘Wendi’. Nilipenda namna Bobi Wine alivyoandika muziki wake,” alisema.

Alimtaja Bobi Wine kuwa stadi katika kutunga nyimbo, akisema hadithi anazoweka katika nyimbo zake humuacha msikilizaji akishangaa.

Kenzo pia alikiri uwezo wa Bebe Cool katika muziki, lakini alisema muziki wake ulikuwa ukivutia zaidi hadhira ya mijini kuliko mitaa ya mabanda alikokulia.

“Bebe Cool daima amekuwa mwanamuziki mzuri, lakini nilitoka kwenye mitaa ya mabanda, na ushawishi wake haukuwa mkubwa huko. Alikuwa zaidi msanii wa mijini, hivyo hatukumkubali sana kwenye mitaa ya mabanda,” alisema.

Share This Article