Lamata ateuliwa mkurugenzi wa Miss Afrikana Tanzania

kwa sasa anahudumu kama Mkurugenzi wa Miss Tanzania Organization.

Marion Bosire
2 Min Read

Leah R. Mwendamseke maarufu nchini Tanzania kama Lamata ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa kitaifa wa shindano la ulimbwende barani Afrika la Miss Afrikana.

Tangazo hilo liliwekwa kwenye akaunti rasmi za Miss Afrikana kwenye mitandao ya kijamii na kuambatanishwa na ujumbe wa kumkaribisha kwenye familia ya shindano hilo.

“Tunajivunia kumkaribisha rasmi Leah R. Mwendamseke kama Mkurugenzi wa Kitaifa wa Miss Afrikana Tanzania”, ilianza taarifa hiyo ikiendelea kumtaja Leah kama kiongozi anayeheshimika katika sekta ya ubunifu nchini Tanzania.

Ametajwa pia kuwa mjasiriamali na mtaalamu wa burudani, akiwa na uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika uongozi wa ubunifu, uendelezaji wa chapa, usimulizi wa hadithi, uzalishaji na ukuzaji wa vipaji.

Leah kwa sasa anahudumu kama Mkurugenzi wa Miss Tanzania Organization, ambapo anatoa uongozi wa kimkakati katika kuunda dira ya shirika, chapa yake, ushirikiano na wadau, pamoja na kuongeza athari zake kitaifa.

Leah pia ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lamata Village Entertainment, kampuni ya ubunifu na uzalishaji inayojikita katika kutengeneza maudhui bora ya filamu na televisheni kutoka Tanzania, huku ikiunda fursa kwa vipaji vya ndani na kuonyesha ubunifu na utamaduni wa Tanzania.

Shindano la Miss Afrikana limeanzishwa na mlimbwende wa asili ya Ghana Abena Akuaba, mshikilizi wa taji la Miss Grand International mwaka 2020 na lile la Miss Grand USA mwaka 2020.

Kulingana na maelezo kwenye akaunti za mitandao ya kijamii, onyesho la kwanza la shindano hilo litafanyika Novemba 11, 2027.

Share This Article