Ray Signature azungumzia safari yake katika muziki

Anaamini urafiki anaojenga njiani pamoja na changamoto na makosa vimechangia pakubwa kuboresha sauti yake na mtazamo wake kama msanii.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji na mtunzi wa nyimbo Ray Signature kutoka Uganda, amefunguka kuhusu jinsi amekua tangu mwanzo wa safari yake ya muziki. 

Anasisitiza kuhusu ukuaji, mafunzo aliyopata na urithi anaohisi anajenga ndani ya tasnia.

Alibainisha kwamba kuwa katika biashara ya muziki kunaweka msanii katika mazingira ya kukutana na watu mbalimbali na kupitia uzoefu tofauti ambao hatimaye huunda sanaa yake na maendeleo yake binafsi.

Kulingana naye, urafiki anaojenga njiani pamoja na changamoto na makosa vimechangia pakubwa kuboresha sauti yake na mtazamo wake kama msanii.

“Unapokuwa kwenye biashara hii, unakutana na watu wengi na kupata marafiki wengi njiani. Unajifunza mengi, na bila shaka unafanya makosa.” Alisema Ray.

Mwimbaji huyo alifichua kuwa moja ya mafanikio anayojivunia zaidi ni mchango anaohisi ameutoa katika tasnia ya muziki, hasa katika utunzi wa nyimbo, sehemu ambayo anaamini athari yake imekuwa kubwa.

Ray Signature pia alitaja hatua nyingine muhimu katika kazi yake, uzinduzi wa tukio lake la kila mwaka la muziki wa moja kwa moja linaloitwa “A Night With Ray Signature.”

Toleo la kwanza Disemba mwaka jana, lilifanikiwa, jambo lililompa motisha kulifanya kuwa tukio la kila mwaka.

“Niliamua kuanza kufanya onyesho kila mwaka. Toleo la kwanza la lilifanyika Disemba iliyopita na lilikuwa la mafanikio. Ni jambo ninalopanga kuendelea nalo kila mwaka,” aliongeza.

Kadri anavyoendelea kukua kimuziki, Ray Signature anaendelea kuzingatia kujenga urithi wa kudumu kupitia muziki wenye maana, maonyesho ya moja kwa moja, na malezi ya vipaji kupitia utunzi wa nyimbo.

Share This Article