Yung Mulo atishia kuchukua hatua za kisheria

Vyombo vya habari vilichapisha taarifa zilizomhusisha na mhalifu aliyehukumiwa kifungo cha miaka 130 jela.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Lubega Kassim maarufu kama Yung Mulo, ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vyombo vya habari nchini humo.

Hii ni baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha taarifa zilizomhusisha na mhalifu aliyehukumiwa kifungo cha miaka 130 jela.

Mkanganyiko ulitokea wakati mhalifu aliyepatikana na hatia alijitambulisha kama “Young Mulo” na kuhukumiwa kifungo cha miaka 130, huku baadhi ya taarifa za vyombo vya habari zikishindwa kutaja jina lake halisi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kuamini kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amekamatwa, kuhukumiwa na kufungwa.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Yung Mulo alifafanua kuwa sio yeye alipatikana na hatia na kuhukumiwa, na kwamba hajawahi kuhusishwa na kesi hiyo ya uhalifu.

Alisema taarifa hizo zimesababisha mkanganyiko miongoni mwa mashabiki zake, wasanii wenzake na umma kwa ujumla, wakati ambapo yeye anaendelea kujikita katika kutangaza tamasha yake ijayo Oktoba 9 huko Munyonyo.

Alihoji kwa nini baadhi ya taarifa hazikutaja jina halisi la mtu aliyepatikana na hatia, akisema kutofanya hivyo kumeleta mkanganyiko usio wa lazima.

Yung Mulo alisisitiza kuwa taarifa hizo zimechafua taswira yake na kuleta dhana potovu kwamba anatumikia kifungo kirefu gerezani.

Amesema atakusanya taarifa hizo pamoja na ushahidi mwingine huku akifikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vyombo vya habari anavyoamini vilipotosha utambulisho wake.

Share This Article