Wabunifu wa Afrika wabadilishana maarifa Kigali

Waandaaji wanataka kongamano hilo liandaliwe kila baada ya miaka miwili na hatimaye kuhusisha shule za sanaa kote Afrika Mashariki.

Marion Bosire
2 Min Read
Celine Fatoux Hagoye, Mwanzilishi wa Hang'art Africa

Wabunifu kutoka Rwanda na maeneo mbalimbali barani Afrika walikutana jijini Kigali wikendi kwa kongamano muhimu.

Kongamano hilo lililopatiwa jina la ‘Creative Talks’, la siku tatu lililenga kuimarisha mabadilishano ya maarifa ya kisanii, malezi ya vipaji na ushirikiano miongoni mwa wabunifu barani humu.

Warsha hiyo ilifanyika Septemba 11 hadi 13, 2026, katika taasisi ya Français na L’Espace, waandalizi wakiwa Hang’Art Africa, shirika huru lililoanzishwa na Celine Fatoux Hagoye kuunganisha wasanii kutoka mifumo mbalimbali ya ubunifu.

Warsha hiyo iliwakutanisha wabunifu katika nyanja za sanaa za kidijitali, uchoraji, upigaji picha, mitindo na dansi.

Miongoni mwa walioshiriki ni mchoraji wa Kenya Velma Rosai, mpiga picha na mtengenezaji filamu kutoka Nigeria Stephen Tayo na mcheza densi Daniel Ahifon.

Wasanii wa Rwanda waliojumuika ni pamoja na msanii wa sanaa za kidijitali Dolph Banza, mpiga picha Serrah Galos, mcheza densi Eya Khalifa na msanii Maurice de Bone.

Hagoye alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wasanii wa ndani kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa wabunifu wenye uzoefu wa kimataifa, huku ukiwapa vijana nafasi ya kushirikisha changamoto, mawazo na matarajio yao.

Kwa Banza, kukutana ana kwa ana kumetoa fursa ambayo mitandao ya kijamii haiwezi kutoa kwa urahisi ambayo ni mazungumzo ya maana kati ya wasanii na hadhira.

Alisema mtagusano wa mtandaoni mara nyingi huishia katika likes, emoji na kushirikishwa kwa kazi, huku mikutano ya ana kwa ana ikiruhusu majadiliano ya kina na majibu yenye kujenga.

Tayo alisema mpango huo unaweza kuimarisha uhusiano kati ya wabunifu katika miji kama Kigali, Nairobi, Lagos na Abidjan.

Rosai alisema kukutana na wasanii kutoka tamaduni tofauti kunatoa msukumo mpya na fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za ubunifu.

Hagoye alisema waandaaji wanatarajia kuandaa kongamano hilo kila baada ya miaka miwili na hatimaye kuhusisha shule za sanaa kote Afrika Mashariki.

Share This Article