Nwagi aomba mashabiki kuheshimu faragha ya watu maarufu

Alisema kuwa kuwa mtu maarufu hakumaanishi kwamba huwa yuko tayari muda wote kuzungumza na mashabiki au kupiga nao picha.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa Uganda, Winnie Nwagi, amewaomba mashabiki kuheshimu faragha ya watu maarufu.

Nyota huyo anasema nao pia huwa na siku ambazo hawajisikii kuwa mbele ya kamera, kupiga picha au kutagusana na watu.

Akizungumza katika kipindi cha mtandaoni cha mwanamuziki mwenzake Sheebah Karungi kiitwacho ‘Let’s Talk About It’, Nwagi alisema kuwa kuwa mtu maarufu hakumaanishi kwamba huwa yuko tayari muda wote kuzungumza na mashabiki au kupiga nao picha.

Alieleza kuwa kuna siku ambazo hata yeye mwenyewe huwa hajisikii kupiga picha yake, hivyo maombi ya ghafla kutoka kwa mashabiki yanaweza kumweka katika hali mbaya.

Nwagi alisema baadhi ya mashabiki huwafuata watu maarufu hasa kwa lengo la kupata picha za kuweka kwenye mitandao ya kijamii, bila kuzingatia jinsi msanii anavyojisikia wakati huo.

Maoni yake yaliungwa mkono na Sheebah, aliyewaonya mashabiki na wanablogu dhidi ya kuwarekodi wasanii bila kuzingatia madhara ambayo maudhui hayo yanaweza kuwasababishia.

Sheebah alisema wanamuziki hutumia miaka mingi kujenga taswira zao hadharani, lakini hilo halimaanishi kuwa huwa wakamilifu au wako tayari muda wote kuonekana mbele ya kamera.

Alisema wasanii wana mapungufu na siku mbaya, hivyo video zinazorekodiwa bila kuzingatia hali zao zinaweza kuwaonyesha kwa namna isiyolingana na taswira waliyojijengea kwa miaka.

Wasanii hao waliwataka mashabiki kuwa na uelewa zaidi wanapowafuata watu mashuhuri, wakisisitiza kuwa mastaa wanastahili nafasi binafsi na heshima licha ya kuwa watu wa hadhara.

Share This Article