Matete avuta kumbukumbu ya baada ya ushindi wa TPF 5

Alizungumzia jinsi alipatiwa mlinzi wa kibinafsi hali iliyobadili mtindo wake wa maisha.

Marion Bosire
2 Min Read

Mhubiri na mwimbaji wa nyimbo za injili Ruth Matete amevuta kumbukumbu ya maisha yake yalivyokuwa punde baada ya kutangazwa mshindi wa shindano la uimbaji la Tusker Project Fame, TPF awamu ya 5.

Katika akaunti yake ya Facebook, Ruth ambaye kwa sasa anaishi nchini Canada, alichapisha picha ya siku hiyo alipotangazwa mshindi akiwa na mwanamke fulani na mlinzi wa kibinafsi nyuma yake.

“Huyu alianza kazi punde baada yangu kutangazwa mshindi wa Tpf 5,” aliandika Ruth akimrejelea mlinzi huyo, akiongeza kwamba mkataba alioingia kufuatia ushindi ulimpa mlinzi wa kibinafsi.

Kulingana naye, kipindi hicho alipata ugumu kidogo kubadili mtindo wake wa maisha na kuwiana na mahitaji ya ulinzi huo wa kibinafsi.

Anasema kwamba hakuwa anaruhusiwa kwenda popote bila mpango wa mapema, ambapo alihitajika kila jioni, kumpa mlinzi huyo ratiba yake ya shughuli ya siku itakayofuata.

“Haungetoka nyumbani kabla hajafika. Kwa hivyo anahitaji kufahamu muda wako wa kuamka. Kwa sababu unapofungua jicho asubuhi, anachukua usukani. Chochote kikikutokea atawajibishwa,” alielezea Matete.

Wakati mwingine angemkatizia muda wa kukaa katika sehemu zilizojaa watu kwa kuhofia usalama wake na kwamba angesafiri naye kwenye gari moja kila mara.

Aliongeza kwamba nyakati zingine mlinzi huyo angemshauri dhidi ya kuenda sehemu fulani ambazo angehisi sio salama na kumpendekezea sehemu mbadala.

Share This Article