Murkomen azungumzia usalama katika ziara ya Isiolo

Alikuwa katika eneo hilo, kushiriki mchango wa kuwawezesha wanawake na kusaidia vyama vya wanafunzi

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, amezungumzia vipaumbele vya usalama na maendeleo ya oparesheni za usalama katika eneo la Oldonyiro, Kaunti ya Isiolo.

Murkomen alikuwa katika eneo hilo, kushiriki mchango wa kuwawezesha wanawake na kusaidia vyama vya wanafunzi.

Murkomen, aliyekuwa ameandamana na Seneta Fatuma Dullo, alisema mpango huo ulikutanisha makundi yanayowakilisha wanawake zaidi ya 2,000 na kusaidia wanafunzi 300 wa vyuo na vyuo vikuu kutoka Eneo Bunge Dogo la Oldonyiro.

Pia alifanya mazungumzo na wawakilishi wa jamii kutoka Isiolo na kaunti jirani kuhusu changamoto za usalama na vipaumbele vya maendeleo.

Waziri alisema operesheni za kukabiliana na wizi wa mifugo, njia za usafirishaji haramu, maeneo ya kuuza pombe haramu, dawa za kulevya na ujangili, zimepata mafanikio.

Alisema serikali inaendelea kuimarisha polisi, kusogeza huduma za kiutawala karibu na wananchi na kuboresha makazi pamoja na mazingira ya kazi ya maafisa wa usalama.

Kuhusu maendeleo, Murkomen alisema serikali inaratibu juhudi za kuboresha barabara na madaraja, kupanua huduma ya umeme, kushughulikia masuala ya makazi na ardhi, kuongeza ajira kwa vijana, na kuboresha vituo vya TVET.

Alisisitiza pia umuhimu wa kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali, ikiwemo vitambulisho vya kitaifa, ili kuwawezesha vijana kupata fursa na kutekeleza haki zao za kiraia.

Share This Article