Mfanyakazi wa zamani wa KenGen ahukumiwa kisa vyeti bandia

David Mogire Nyabuti alipatikana na hatia ya kupata mali ya umma kwa njia ya udanganyifu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mfanyakazi wa zamani wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Kenya, KenGen amehukumiwa baada ya kupatikana na hatia inayohusiana na vyeti.

Jamaa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 11 gerezani au faini ya zaidi ya shilingi milioni 16, baada ya kupatikana na hatia ya kutumia vyeti bandia vya kitaaluma na ulemavu.

David Mogire Nyabuti alipatikana na hatia na Mahakama ya Kupambana na Ufisadi baada ya upande wa mashtaka, ukiongozwa na Naomi Isoe, kuthibitisha kuwa alipata mali ya umma kwa njia ya udanganyifu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Hakimu Mkuu Mwandamizi C. Okore aliamuru Nyabuti alipe milioni 14.946 kama fidia kwa mishahara na marupurupu aliyopata kwa njia ya udanganyifu.

Pia alitozwa faini ya shilingi 900,000 na nyingine ya shilingi 200,000 kwa kila moja ya mashtaka mawili ya kuwasilisha nyaraka za uongo. Hukumu hizo zitatekelezwa kwa wakati mmoja.

Nyabuti alifanya kazi KenGen kuanzia Agosti 2003 hadi Septemba 2018, alipowasilisha ombi la kujiuzulu.

Mahakama ilielezwa kuwa alitumia cheti bandia cha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne, KCSE kilichoonyesha alama ya wastani ya C-, licha ya kupata D- katika mtihani wa KCSE wa 1994 katika Shule ya Sekondari ya St Paul’s Igonga.

Pia alipata kwa njia ya udanganyifu cheti cha ulemavu, kilichomwezesha kunufaika na misamaha ya kodi kati ya Julai 2014 na Septemba 2018.

Nyabuti alijiuzulu baada ya KenGen kumtaka kuwasilisha vyeti vyake halisi vya kitaaluma.

Share This Article