Mama Fatma Karume kuzikwa leo alasiri

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alisema mazishi yatafanyika katika makaburi ya familia.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwili wa Mama Fatma Karume, mke wa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, utazikwa leo alasiri.

Haya ni kulingana na tangazo lililotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Katika tangazo lake, Abdulla alielezea kwamba mazishi hayo yatafanyika saa 10 alasiri katika makaburi ya familia.

Mama Fatma Karume alifariki jana Septemba 21 2026 akiwa na umri wa miaka 97, huku viongozi mbali mbali wa Tanzania wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakimwomboleza.

Rais Samia katika ujumbe wake alisema kifo hicho kimeacha pengo kwa familia na Taifa kwa jumla, kwani Mama Fatma, alikuwa sehemu muhimu ya historia adhimu ya Zanzibar kuanzia nyakati za harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Daima tutaendelea kukumbuka, kuenzi na kuheshimu mchango wake katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wetu, pamoja na kuchochea mandeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya Taifa letu,” alisema Rais Samia.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, naye alitoa salamu za pole kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na familia, ndugu na jamaa, kufuatia kifo cha Mama Fatma Karume.

Naye vile vile alimtaja marehemu Mama Fatma Karume kuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar na Tanzania.

Share This Article