Familia ya mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu imetangaza kwamba kakake Tundu Allute Mughwai, atazikwa baada ya Tundu kusomewa hukumu yake.
Mazishi hayo ya Mughwai aliyefariki usiku wa kuamkia jana Novemba Mosi, 2026, yamepangiwa kufanyika nyumbani kwao kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida.
Kiongozi huyo wa CHADEMA amekuwa kizuizini tangu mwezi Aprili mwaka uliopita ambapo anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, akisubiri kusomewa hukumu Novemba 6, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Ndugu mwingine wa Tundu Lissu aitwaye Vincent alisema kwamba familia imeamua kufanya msiba wa kaka yao Alute, baada ya Ijumaa ijayo, kutokana na tukio muhimu la hukumu ya kesi ya uhaini, inayomkabili ndugu yao Tundu.
“Tumepanga mazishi ya kaka Alute yatafanyika Singida. Tunatarajia tutasukuma mbele mazishi ili Ijumaa, Novemba 6 2026, wanafamilia tuweze kuwepo Dar es Salaam kuhudhuria hukumu ya kesi ya ndugu yetu Tundu,” alifafanua.
Alute alikuwa akiugua kwa muda mrefu ambapo siku za hivi karibuni alilazwa katika Hospitali moja jijini Arusha na kuanzia juzi alizidiwa kabla ya kukumbana na mauti.