Mtihani wa maandishi wa kidato cha nne waanza

Msimu wa mitihani ya KCSE 2026 ulianza Oktoba 19 kwa mitihani ya maongezi, vitendo na masomo yenye watahiniwa wachache.

Marion Bosire
2 Min Read

Watahiniwa zaidi ya milioni moja wameanza kufanya mtihani wa Kidato cha Nne, KCSE mwaka 2026, huku leo Jumatatu ikiashiria mwanzo wa mitihani mikuu ya maandishi kote nchini.

Jumla ya watahiniwa 1,048,355 walijisajili kufanya mtihani wa mwaka huu, mara ya kwanza katika historia ya mitihani ya kitaifa nchini Kenya kwa idadi ya watahiniwa wa KCSE kuzidi milioni moja.

Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alitangaza takwimu hizo mapema leo, baada ya kushuhudia kufunguliwa kwa kasha la mitihani la Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya, KNEC katika ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti huko Borabu, Kaunti ya Nyamira.

Idadi hiyo inaonyesha ongezeko la asilimia 5.27 ikilinganishwa na watahiniwa 995,860 waliojisajili mwaka 2025, huku mwaka 2024 ukiwa na watahiniwa 965,172.

Msimu wa mitihani ya KCSE 2026 ulianza Oktoba 19 kwa mitihani ya maongezi, vitendo na masomo yenye watahiniwa wachache, ambayo tayari yamefanywa na watahiniwa waliojisajili kwa masomo husika.

Mitihani mikuu ya maandishi imeanza leo Jumatatu, ambapo watahiniwa walipangiwa kufanya Karatasi ya Kwanza ya Kiingereza asubuhi na Karatasi ya Kwanza ya Kemia alasiri.

Mitihani hiyo itaendelea hadi Novemba 20 na inasimamiwa katika zaidi ya vituo 10,000 kote nchini.

Ogamba alisema serikali imeimarisha usalama wa vifaa vya mitihani ili kuzuia kuvuja kwa mitihani mapema, lakini akaonya kuwa udanganyifu bado ni changamoto.

Share This Article