Knowless Butera ang’aa kwenye tamasha ya Improper Access

Alikuwa msanii mkuu katika toleo la tatu la tamasha ya Improper Access jijini Kigali.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa kike wa Rwanda Knowless Butera, alikuwa msanii mkuu katika toleo la tatu la tamasha ya Improper Access, ambako alitoa burudani ya kusisimua katika hafla hiyo inayolenga kukuza vipaji vya wanawake katika tasnia ya burudani.

Tamasha hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya matukio ya Blackout Inc. yenye makao yake jijini Kigali, ilifanyika katika ukumbi wa Camp Kigali Oktoba 31, ikiwa na orodha ya wapiga muziki wanawake pekee.

Butera, aliyekuwa mwimbaji pekee katika hafla hiyo, alipanda jukwaani majira ya saa 5:40 usiku, akianza na wimbo wake “Sweet Mutima”, kabla ya kuimba nyimbo nyingine maarufu zikiwemo “Sinzakwibagirwa”, “Akantu”, “Umutima” na “Ngufite Urampagije”.

Wakati mmoja mashabiki walimwomba aimbe “Rubanda”, wimbo uliotengenezwa upya kwa ushirikiano na Abdul Makanyaga. Ingawa haukuwa kwenye orodha yake ya nyimbo alizopanga kuimba, Butera alikubali ombi hilo na kuwafanya mashabiki kuimba pamoja naye kwa shangwe.

Butera alihitimisha onyesho lake majira ya saa 7:30 usiku, akiwashukuru waandaaji kwa kuunda fursa kwa wanawake katika tasnia ya burudani na kuhimiza umma kuunga mkono mipango hiyo.

Tamasha ya Improper Access ilizinduliwa mwaka 2024 na awali ilikuwa ikishirikisha wasanii kutoka mataifa mbalimbali lakini toleo lake la tatu lilijikita kikamilifu katika vipaji vya ndani.

Hafla hiyo inadhamiriwa kuwapa wasanii wa kike na wapiga muziki yaani ma-DJ wa kike wa Rwanda fursa zaidi za kukuza taaluma zao.

Share This Article