Kundi maarufu la ngoma za kitamaduni la Inganzo Ngari nchini Rwanda linajiandaa kusherehekea miaka 20 ya kukuza na kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa taifa hilo.
Limeandaa amasha kubwa itakayofanyika Novemba 21 katika ukumbi wa BK Arena, jijini Kigali.
Tamasha hiyo ambayo wameipa jina la “Umurage w’Intore” itakuwa sehemu ya maadhimisho ya miongo miwili ya kundi hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 2006 na takriban wanafunzi 20 wa vyuo vikuu jijini Kigali.
Lengo la kuunda kundi hilo lilikuwa kuhamasisha vijana kukumbatia ngoma za kitamaduni na kupinga dhana kwamba sanaa hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwa ajili ya wazee pekee.
Kwa mujibu wa mkurugenzi na mkufunzi mkuu wa kundi hilo, Serge Nahimana, Inganzo Ngari imekua kwa kiasi kikubwa licha ya changamoto na ukosoaji wa awali, huku idadi ya wanachama hai ikizidi 100.
Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni ushindi katika mashindano ya kimataifa nchini Uhispania mwaka 2008, ambapo lilitambuliwa kuwa kundi bora zaidi la ngoma duniani.
Nahimana alisema kundi hilo pia limebadilisha maisha ya wanachama wake, huku baadhi wakitumia mapato ya maonyesho kugharamia masomo ya vyuo vikuu na kujenga nyumba.
Tamasha ijayo itawapa mashabiki fursa ya kufahamu historia ya Rwanda kupitia ngoma za kitamaduni zitakazoonyesha urithi wa taifa hilo katika uhalisia wake.
Mwimbaji Ruti Joel atakuwa msanii mgeni maalumu, huku wasanii wengine wakitarajiwa kutangazwa baadaye.