Idara ya mahakama yaandaa siku ya michezo, utamaduni na talanta

Tukio hilo lilikutanisha majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Marion Bosire
1 Min Read

Jaji Mkuu Martha Koome jana aliongoza idara ya Mahakama nchini kuadhimisha Siku ya Michezo, Utamaduni na Vipaji, yenye kaulimbiu ya “Kusawazisha Ustawi, Uadilifu na Huduma”.

Tukio hilo lilikutanisha majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha mshikamano, kukuza vipaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mwanariadha mashuhuri na bingwa wa mbio za marathoni, Kanali Dkt. Paul Tergat, alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo iliyojumuisha shughuli mbalimbali za michezo ya ndani na nje, maonyesho ya utamaduni na vipaji.

Timu kutoka maeneo 16 zilishiriki shughuli hizo, zikitoa fursa kwa wafanyakazi kushirikiana nje ya majukumu yao ya kawaida.

Msajili Mkuu wa Mahakama, Winfridah Mokaya, pia aliongoza mpango maalum wa maonyesho yenye kaulimbiu ya ‘Mabadiliko ya Kijamii Kupitia Upatikanaji wa Haki’.

Mpango huo ulilenga kukuza maadili na misingi ya taasisi hiyo huku washiriki wakionyesha kwa ubunifu jinsi mpango wa upeleka huduma za mahakama karibu na wananchi unaeleweka na kutekelezwa mahakamani na katika ngazi ya mashinani.

Mahakama ilisema kuwa mahakama zote ziliendelea kutoa huduma bila usumbufu wakati wa hafla hiyo.

Tergat aliambia washiriki kwamba mapumziko, burudani na mazoezi ni muhimu katika kujenga wafanyakazi wenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia jamii yenye haki.

Share This Article