Rais William Ruto amesema raia wa Kenya ambao walisajiliwa kwa shughuli za kijeshi nchini Urusi watarejeshwa nyumbani.
Kiongozi wa taifa alisema wamekubaliana na mwenyeji wake wa Urusi Vladimir Putin kwamba hakuna raia yeyote wa Kenya atasajiliwa tena kwenye vikosi vya ulinzi nchini Urusi.
Kwenye mkutano na rais Putin leo Ijumaa Jijini Moscow, Ruto alisema alimfahamisha mwenyeji wake kuhusu hatua ya kumpeleka mwakilishi wa kijeshi wa Kenya kwenye ubalozi wa Kenya Jijini Moscow, ili kufanikisha hatua ya kuwarejesha nyumbani Wakenya hao.
“Mwakilishi huyo wa kijeshi atashirikiana kwa karibu na Wizara ya Ulinzi ya Russia kutekeleza mchakato wa kuwafidia Wakenya na kuwasaidia kurejea nyumbani,” alisema Rais Ruto.
Rais Putin alijitolea kuunga mkono upanuzi wa afisi za Umoja wa Mataifa Jijini Nairobi, ambayo ndiyo ya pekee katika mataifa yanayoendelea.
Kulingana na Rais Ruto, viongozi hao wawili walikubaliana kujadili kuhusu makubaliano ya leba yatakayowawezesha Wakenya kufanya kazi na kuishi nchini Urusi.
Wakati huo huo, Rais Ruto alimkaribisha Rais Putin kuzuru Kenya.