Hazina ya Kitaifa ya Serikali Kuhusu Hatua za Kimakusudi, NGAAF, imetakiwa kupanua mipango inayolenga kuwezesha wanawake kiuchumi.
Wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Hazina Zilizogatuliwa walisema hazina hiyo inapaswa kuimarisha mipango inayosaidia kuboresha maisha ya wanawake na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu katika jamii.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NGAAF alisema hazina hiyo imefanikiwa pakubwa katika kaunti mbalimbali, kwa kuzingatia miradi ya makundi ya wanawake inayozalisha mapato na vituo vya kuhudumia waathiriwa wa Ukatili wa Kijinsia, GBV.
NGAAF iliwasilisha taarifa zake mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Gideon Mulyungi, kwa ajili ya kuchunguzwa kwa ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za hazina hiyo mwaka 2024/2025.
Afisa Mkuu Mtendaji alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kaunti mbalimbali, akitaja miradi ya visima na vituo vya GBV vilivyoanzishwa kutoa makazi na msaada kwa wanawake na watoto walioathiriwa na ukatili.
Kamati hiyo ilihimiza NGAAF kuongeza mipango kama hiyo ya uwezeshaji, ikibainisha kuwa miradi inayotekelezwa na wanawake, inatoa fursa kwao kuboresha maisha yao na kuimarisha uhuru wao wa kiuchumi.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mulyungi, alihimiza NGAAF kuhakikisha rasilimali zake zinatumika ipasavyo ili kufikia malengo yaliyowekwa, akimpongeza Afisa Mkuu Mtendaji kwa kuwa na masuala machache ya ukaguzi yaliyoibuliwa katika mapitio ya hesabu za hazina hiyo.