Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini, EPRA, imedumisha bei za mafuta kwa kipindi cha Novemba 15 hadi Desemba 14, 2026.
Hatua hii inawapa nafuu wanaotumia bidhaa za mafuta licha ya kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la kimataifa.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumamosi, Novemba 14, 2026, EPRA ilitangaza kuwa bei za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zitasalia bila mabadiliko kote nchini kwa siku 30 zijazo.
Nairobi, lita moja ya Petroli itaendelea kuuzwa kwa shilingi 226.96, Dizeli kwa shilingi 227.76 na Mafuta ya Taa kwa shilingi 219.87.
Uamuzi huo umeafikiwa licha ya kuongezeka kwa wastani wa gharama za uagizaji wa bidhaa za mafuta kati ya Septemba na Oktoba 2026.
Gharama ya Petroli ilipanda kwa asilimia 6.11, Dizeli kwa asilimia 6.73, huku Mafuta ya Taa yakiongezeka kwa asilimia 0.71.
Ili kuwalinda watumiaji dhidi ya ongezeko la gharama, serikali imetenga shilingi bilioni 4.6 kutoka kwenye Hazina ya Ushuru wa Maendeleo ya Petroli ili kudhibiti bei za mafuta katika kipindi hiki.
EPRA ilisema bei hizo zinajumuisha Ushuru wa Ongezeko la Thamani, VAT, wa asilimia 8, kulingana na sera ya serikali ya kuwalinda wananchi dhidi ya athari za kupanda kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa.