Semakula akutanisha nyota wa muziki Uganda

Jose Chameleone, Juliana Kanyomozi, Stecia Mayanja, Rema Namakula na wengine walikutana kwenye tamasha yake ya siku ya kuzaliwa.

Marion Bosire
1 Min Read

Tamasha ya kusherehekea miaka 50 ya mwanamuziki wa Uganda Mesach Semakula iliwakutanisha baadhi ya nyota wakubwa wa muziki nchini humo.

Hafla hiyo vile vile ilikumbwa na malalamiko ya mashabiki kuhusu gharama za viti, maegesho ya magari na changamoto za uandaaji.

Tamasha hiyo iliyofanyika Ijumaa katika ukumbi wa Kingdom Kampala, iliwahusisha wasanii Jose Chameleone, Juliana Kanyomozi, Stecia Mayanja na Rema Namakula, miongoni mwa wengine waliohudhuria kumpongeza Semakula.

Semakula aliwafurahisha mashabiki kwa vibao vyake maarufu vikiwemo “Kankutendeleze”, “Thank You”, “Bwagamba”, “Bekengere” na “Mummy”, huku mashabiki wakiimba pamoja naye.

Pia aliwakumbuka wanamuziki wenzake waliofariki, akiwemo Moses Matovu, mwanzilishi wa bendi ya Afrigo na Paul Kafero, kwa kuwaimbia nyimbo maalumu za kuwaenzi.

Hata hivyo, sherehe hizo zilikatizwa kwa muda na mvua kubwa iliyowalazimu waandaaji, Fenon Events, kuzima vifaa vya sauti na mwanga saa 3:45 usiku. Burudani iliendelea tena saa 5 usiku.

Kufuatia malalamiko ya mashabiki kuhusu gharama za viti na maegesho pamoja na changamoto za uzalishaji, Semakula aliomba radhi, akisema alitumia hadi Shilingi milioni 300 za Uganda kuandaa tamasha hiyo.

Alisisitiza kuwa hakukuwa na nia ya kuwanyonya mashabiki, bali kuwapa sherehe ya kukumbukwa katika siku yake ya kuzaliwa.

Share This Article