Serikali itatumia kitita cha shilingi bilioni 17, kujenga nyumba za bei nafuu, masoko na mabweni ya wanafunzi katika kaunti ya Trans Nzoia.
Akiwa kwenye ziara ya kikazi katika kaunti hiyo, Rais William Ruto alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.5, zitatumika kwa ujenzi wa masoko 15 ya kisasa, hatua itakayowezesha mazingira bora ya kikazi kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Alikagua ujenzi unaoendelea wa soko la kisasa la Kiminini, litakalowakimu wafanyabiashara 500. Ujenzi wa mradi huo unaogharimu shilingi milioni 181, umekamilika asilimia 50, na unatarajiwa kukamilika kufikia mwezi Disemba 2026.
Wakati huo huo, alizindua ujenzi wa barabara ya Kiminini-Mitoto-Ndalu-Brigadier katika kaunti ya Trans Nzoia, itakayogharimu shilingi milioni 500.
Tutaongeza shilingi bilioni moja zaidi kukamilisha ujenzi huo,” alisema Rais Ruto.
Aidha, alisema serikali inawekeza shilingi bilioni saba kwa upanuzi wa barabara ya Maili Tisa-Kitale.
“Kote nchini, tumewekeza shilingi bilioni 28 kwa ujenzi wa kilomita 270 za barabara,” aliongeza kiongozi wa taifa.