Kenya yathibitisha kisa cha pili cha ugonjwa wa Ebola

Mkurugenzi wa Afya Dkt. Patrick Amoth, alidokeza kuwa mgonjwa huyo tayari alikuwa karantini na alianza kuonyesha dalili za ugonjwa huo Oktoba 13, 2026.

Tom Mathinji
1 Min Read
Dr. Patrick Amoth - Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini Kenya.

Wizara ya Afya nchini Kenya imethibitisha kisa cha pili cha ugonjwa wa Ebola, ikisema mwathiriwa huyo mwenye umri wa miaka 39 aliyekuwa karantini, ni jamaa wa karibu wa mgonjwa wa kwanza.

Kupitia kwa taarifa Jumatano jioni iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini Kenya  Dkt. Patrick Amoth, mgonjwa huyo tayari alikuwa karantini na alianza kuonyesha dalili za ugonjwa huo Oktoba 13, 2026.

Kulingana na Dkt. Amoth,  mgonjwa huyo alipata ongezeko la joto mwilini, maumivu ya viungo vya mwili na uchovu mwilini, na kusababisha maafisa wa karantini kumtenga na kuchukua sampuli.

“Sampuli hizo zilipelekwa katika Maabara ya Kitaifa na Ile ya Taasisi ya Uchunguzi wa Matibabu (KEMRI)-CDC, na kupatikana kuwa na ugonjwa huo,” alisema Amoth.

Amoth alisema ugunduzi wa mapema ulifanikishwa na hatua ya haraka ya karantini , akiongeza kuwa maambukizi hayo mawili yaliyonakiliwa nchini Kenya hayana ushahidi wa maambukizi katika jamii nzima.

Kufikia sasa, Kenya imenakili visa viwili vya Ebola, huku mtu mmoja akifariki kutokana na makali ya ugonjwa huo.

Share This Article