Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewakamata watu wawili wanaodaiwa kuitisha na kupokea pesa kutoka kwa mtu anayechunguzwa na tume hiyo.
Walionaswa na mkono mrefu wa sheria ni Hellen Hashiali Masinde na Violet Ndakwa, wote wakazi wa kaunti ya Kakamega.
Nao wanaripotiwa kudai kuwa wana ‘mitandao’ ndani ya EACC wanayoweza kutumia kushawishi matokeo ya uchunguzi huo.
Washukiwa wanadaiwa kuitisha shilingi 100,000 na walikamatwa jana Jumatano baada ya kupokea shilingi 30,000.
Wawili hao wanadaiwa kuwa sehemu ya kundi la walaghai wanaoendesha shughuli zao eneo la Magharibi, ama kwa kusingizia kuwa maafisa wa EACC au kwa kudai kuwa wana ushawishi juu ya uchunguzi unaoendeshwa na tume hiyo.
Waliandikisha taarifa katika afisi ya kanda ya Magharibi ya EACC na kisha kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma Central wakisubiri kukamilishwa kwa uchunguzi na kisha kufikishwa mahakamani.