Joseph Kabila achaguliwa kiongozi wa muungano wa waasi DRC

Muungano huo umesema utatimiza lengo la kuiondoa serikali madarakani, kwa njia zote, ikiwemo kutumia nguvu.

Marion Bosire
2 Min Read
Aliyekuwa Rais wa DRC Joseph Kabila.

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Joseph Kabila, ametangazwa kuwa kiongozi wa muungano mpya wa waasi unaolenga kuiondoa serikali madarakani.

Muungano huo unaoitwa Front for the Refoundation of the Nation, FRN, umesema unalenga kuratibu “vikosi vya upinzani” ili kukomesha kile unachokiita “udhalimu” nchini DRC.

Muungano huo umesema utatimiza lengo hilo “kwa njia zote, ikiwemo kutumia nguvu.”

Kutangazwa kwa muungano huo siku ya Jumatatu ni ishara ya wazi zaidi kufikia sasa ya kuhusika moja kwa moja kwa Kabila katika harakati za kijeshi, mwaka mmoja baada ya kuhukumiwa kifo akiwa hayupo mahakamani kwa kosa la uhaini.

Awali, Kabila alikanusha kuhusishwa na kundi la waasi la M23 na serikali ya Congo bado haijatoa maoni kuhusu tangazo hilo.

Claude Ibalanky, mshauri wa muungano huo, alitangaza viongozi wa kundi hilo katika mkutano na wanahabari kwenye makazi ya Kabila mjini Goma, jiji kubwa zaidi mashariki mwa DRC ambalo limekuwa chini ya udhibiti wa M23 tangu mwaka jana.

Video iliyotolewa na kundi hilo ilimuonyesha Kabila akitia saini nyaraka, wakati wa kutangazwa kwa muungano huo, akiwa pamoja na viongozi wengine.

Kiongozi wa M23, Sultani Makenga, atakuwa mmoja wa manaibu wanne wa Kabila katika vuguvugu hilo jipya. Wengine watatu pia wanatoka katika muungano wa AFC-M23, ambao mwaka jana uliteka maeneo mengi ya mashariki mwa DRC yenye utajiri wa madini.

Share This Article