Gavana Waiguru kuwania Urais mwaka 2032

Waiguru alisema wanawake ni sharti wajumuishwe katika meza ya ngazi za juu ya kisiasa.

Tom Mathinji
1 Min Read
Anne Waiguru - Gavana wa Kirinyaga.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, ametangaza azma yake ya kuwania wadhifa wa Urais mwaka 2032, huku akitoa ishara ya kuwa Naibu wa Rais wa Rais William Ruto kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Alisema azma hiyo imechochewa na miaka ambayo amehudumu katika Utumishi wa Umma, na kujitolea kwake kusambaratisha vikwazo vya uongozi wa wanawake  kwa vizazi vijavyo.

Waiguru aliyetangaza hayo siku ya Jumanne wakati wa mkutano wa uongozi wa wanawake wa G7, alisema wanawake ni sharti wajumuishwe katika meza ya ngazi za juu ya kisiasa.

Aliwahimiza wanawake kupigania nafasi yao ya uongozi, akidokeza kuwa kamwe hawapaswi kusubiri kupewa nafasi na viongozi wengine wa kisiasa.

“Nataka kutoa tangazo leo kwamba Anne Mumbi Waiguru atawania Urais wa Jamhuri ya Kenya mwaka 2032,” alisema Gavana huyo ambaye amehudumu wadhifa huo kwa mihula miwili.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, Gavana huyo alitoa wito kwa wanawake kujumuishwa katika mazungumzo za ngazi za juu za kisiasa akisema kuwa wanawake wanapaswa kuonyesha azma yao katika wadhifa wa Naibu Rais.

“Nataka kuweka bayana kwamba, nitashinikiza kujumuishwa kwa wanawake katika meza hiyo, ikiwa ni pamoja na mazungumzo kuhusu wadhifa wa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” alisema Waiguru.

Share This Article