King James kuandaa tamasha Marekani

Msanii huyo wa Rwanda atatumbuiza katika ukumbi wa maonyesho huko Phoenix, Arizona, Novemba 28, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Rwanda James Ruhumuriza maarufu kama King James anapanga kutumbuiza mashabiki zake nchini Marekani anaposherehekea miongo miwili katika tasnia ya muziki.

King James anapangiwa kutumbuiza katika maeneo mbali mbali nchini marekani lakini kufikia sasa amethibitisha uwepo wake katika tamasha moja tu.

Tamasha hiyo itaandaliwa katika ukumbi wa maonyesho huko Phoenix, Arizona, Novemba 28, 2026, huku usimamizi wake ukiendeleza mazungumzo kuhusu maonyesho katika miji mingine ya Marekani kabla ya ziara ya King james kumalizikia Canada.

Kampuni ya kuandaa tamasha nchini Marekani ya Afrohub Music Ent inayomilikiwa na Ernesto Ugeziwe, imesema kwamba tiketi za onyesho hilo zitaanza kuuzwa Septemba 29.

Ziara ya King James Marekani inafuatia maonyesho mawili yaliyojaa katika ukumbi wa BK kabla ya mengine katika miji mbali mbali ya Ulaya.

King James alianza kazi rasmi kama mwanamuziki mwaka 2006 akiwa katika shule ya upili. Alikuza talanta yake kwa kuimba shuleni na hata kanisani.

Mwaka 2008 ndio alizindua wimbo uitwao, “Itinyi” ambao ulipendwa na wengi na hivyo kuongeza umaarufu wake nchini rwanda.

Kufikia 2010, King James alikuwa amejiimarisha sana na kuwa mmoja wa wasanii wakubwa wa muziki nchini Rwanda wakiwemo Tom Close, Meddy na The Ben.

Alisajiliwa na kampuni ya Kina Music mwaka 2010 na mwaka 2011 akatoa albamu ya kwanza iitwayo “Umugisha”, ikifuatiwa na “Umuvandimwe” ya mwaka 2012.

Share This Article