Kindiki aongoza kikao maalum cha maandalizi ya El Niño

Wadau walikubaliana kuharakisha kazi za kuchimba na kusafisha mito, kufungua mifereji iliyozibwa, kukagua njia za kusafirisha umeme na kuimarisha hatua zingine.

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais Kithure Kindiki ameandaa kikao maalum cha maandalizi ya El Niño kujadili hatua za kukabiliana na mafuriko na usimamizi wake katika kaunti za Nairobi na Mombasa.

Kikao hicho kilichofanyika katika makazi rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen, kiliwakutanisha viongozi na mashirika muhimu ya serikali, kama vile Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu nchini, KeNHA, Mamlaka ya Barabara za Mijini Kenya, KURA, Mamlaka ya Barabara za Mashinani Kenya, KeRRA, kampuni ya Umeme ya Kenya Power na Tume ya Mito ya Nairobi.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, wawakilishi kutoka wizara husika pamoja na maafisa kutoka Idara za Serikali za Nishati, Barabara na Maendeleo ya Miji pia walihudhuria kikao hicho.

Wakati wa kikao hicho, walikubaliana kuharakisha kazi zinazoendelea za kuchimba na kusafisha mito, kufungua mifereji iliyozibwa, kukagua njia za kusafirisha umeme na kuimarisha hatua zingine za kupunguza athari za mvua kubwa.

Wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na mafuriko wamehimizwa kuhamia maeneo salama yaliyotambuliwa.

Serikali imesema uhamishaji huo utafanyika kwa utaratibu na kwa kuzingatia utu, huku familia zilizoathirika zikipatiwa chakula, mahitaji yasiyo ya chakula na msaada wa matibabu.

Mamlaka zimesisitiza kuwa uhamishaji huo wa muda ni muhimu kwa ajili ya kulinda maisha na kuwataka wakazi kuzingatia maagizo ya usalama.

Serikali imewahakikishia wakazi wa Nairobi kuhusu dhamira yake ya kupunguza uharibifu unaoweza kusababishwa na mafuriko, wakati taifa likijiandaa kukabiliana na mvua inayotarajiwa ya El Nino.

Share This Article