Tume ya Filamu Kenya, KFC, inaongeza juhudi za kukuza sekta ya ubunifu nchini kwa kuimarisha ushirikiano unaolenga kukuza vipaji na uzalishaji wa kazi za ubunifu katika ngazi ya kaunti.
Wawakilishi wa tume hiyo walifanya mashauriano na Idara ya Utalii, Biashara, Utamaduni na Vyama vya Ushirika vya Kaunti ya Taita Taveta pamoja na Chuo Kikuu cha Taita Taveta, kwa lengo la kutafuta njia za kuongeza fursa kwa wabunifu wa eneo hilo.
Mazungumzo na serikali ya kaunti yalilenga kubadilishana takwimu ili kuboresha mipango, kusogeza fursa za ubunifu karibu na wananchi, kuimarisha ujuzi na kuanzisha vituo vya kukuza vipaji vya ubunifu.
Vituo hivyo vinavyopendekezwa vitatoa mafunzo, ushauri, msaada wa uzalishaji, fursa za ushirikiano na kuwaunganisha wabunifu na wadau wa sekta hiyo, hivyo kuwawezesha kujenga taaluma na biashara endelevu.
Katika Chuo Kikuu cha Taita Taveta, Tume ilijadili namna ya kuunganisha elimu na ukuzaji wa vipaji pamoja na sekta pana ya ubunifu. Wanafunzi tayari wamezalisha kazi mbalimbali za ubunifu, huku Tume ikitaka kuanzishwa kwa majukwaa yatakayowasaidia kuboresha ujuzi, kuonyesha kazi zao na kufikia hadhira pana.
KFC ilisema Taita Taveta ina utajiri wa tamaduni, mandhari, vipaji na hadithi zinazoweza kuchangia uchumi wa ubunifu nchini na kuitangaza kaunti hiyo kama kivutio cha utalii.
Tume hiyo ilisema ushirikiano kati ya serikali, vyuo vikuu, wabunifu na wadau wa sekta utasaidia kujenga mfumo imara wa kukuza vipaji hadi uzalishaji, kufikia hadhira na kupata fursa za kibiashara.