Maafisa wa Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya (KWS) mjini Machakos wamewakamata jumla ya watu 11 ndani ya mwezi mmoja uliopita – 7 wakiwa na pembe za tembo na 4 wakiwa na nyama ya wanyamapori.
Kwa mujibu wa Afisa Msimamizi wa Wanyamapori katika Kaunti Ndogo ya Machakos, Ismael Kiprop, wawili kati yao walikamatwa jana Jumanne mjini Machakos wakisafirisha pembe za tembo kwa kutumia pikipiki.
Pembe hizo zinakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 1.2 na uzito wa kilo 12.
Kiprop amesema kuwa visa vingine vilivyobaki ni pamoja na watu watano waliokamatwa na pembe za tembo zenye thamani ya shilingi milioni 1.3, na watu wanne waliokamatwa na nyama ya wanyamapori.
Ametoa wito kwa wakazi wa Machakos kuwa waangalifu wanaponunua nyama kutokana na kuongezeka kwa uchinjaji haramu wa wanyamapori.
Kati ya watu wawili waliokamatwa jana, mmoja anadaiwa kuwa mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Machakos na wamepangiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao.
Taarifa ya Jonathan Musau