Waziri wa Madini, Uchumi wa Buluu na Masuala ya Bahari, Ali Hassan Joho, ameomboleza kifo cha Dkt. Bwanaheri Omar Lali.
Amemtaja kuwa mtu mashuhuri ambaye mchango wake ulisaidia kuunda sekta ya bahari nchini Kenya na historia ya Bandari ya Mombasa.
Katika ujumbe wake wa rambirambi, Joho alisema Lali alihudumu kwa umahiri kama Kapteni wa Bandari Afrika Mashariki na Meneja wa Uendeshaji katika kampuni ya Inchcape Shipping Services.
Akiwa huko alijitolea katika taaluma yake kwa maendeleo ya usafirishaji wa majini, shughuli za bandari na sekta ya bahari kwa jumla.
Waziri huyo alimtaja marehemu Lali kuwa taasisi, akimsifu kwa utaalamu, uadilifu, nidhamu na kujitolea kwake katika kutekeleza majukumu.
Kwa mujibu wa Joho, Lali alipata heshima kubwa miongoni mwa wafanyakazi wenzake, mawakala wa meli, mabaharia na jamii nzima ya bandari kutokana na uelewa wake mpana wa Bandari ya Mombasa na huduma yake kwa sekta hiyo.
Joho alisema kifo cha Lali kimeacha pengo kubwa katika sekta ya bahari nchini Kenya, huku urithi wake ukiendelea kupitia watu aliowalea kitaaluma, taasisi alizoimarisha na viwango vya kitaaluma alivyosaidia kuweka.
Alitoa rambirambi kwa familia, marafiki, wafanyakazi wenzake katika Inchcape Shipping Services na wadau wote wa sekta ya bahari na bandari.