Ruto azuru Homa Bay, akagua miradi ya maendeleo

Akiwa kaunti hiyo, Rais alikagua ujenzi unaoendelea wa soko la kisasa la Misambi katika eneo bunge la Kabondo-Kasipul ambalo punde litakapomalizika, litatumika na wafanyabiashara 200. 

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto aliendelea na ziara yake ya eneo la Nyanza kwa kutembelea kaunti ya Homa Bay leo Alhamisi, ambako alitoa wito kwa wakazi kuunga mkono serikali jumuishi ili kunufaika na miradi mingi zaidi ya maendeleo. 

Akiwa Homa Bay, Ruto alikagua ujenzi unaoendelea wa soko la kisasa la Misambi katika eneo bunge la Kabondo-Kasipul ambalo punde litakapomalizika, litatumiwa na wafanyabiashara 200.

Ujenzi wa soko hilo umepangwa kumalizika mwezi Novemba.

Ruto akisifia ujenzi unaoendelea wa mamia ya masoko nchini akisema utahakikisha wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao katika mazingira safi.

“Ujenzi unaoendelea wa masoko ya kisasa 600 haujawahi kutokea nchini mwetu na hakuna serikali yoyote imejenga aina hii ya miubndombinu tangu uhuru wetu mnamo mwaka 1963,” alisema Ruto.

“Tunajenga masoko kwa sababu tuliwaahidi Mama Mboga na wafanyabiashara wengine kuwa tutawajengea masoko ya kisasa na safi ya kufanyia kazi. Katika kaunti ya Homa Bay pekee, tunawekeza shilingi bilioni 3.5 kujenga masoko mapya ya kisasa 21.”

Rais Ruto aliyasema hayo wakati akiwa ameandamana na viongozi mbalimbali wa kaunti hiyo, wakiongozwa na Gavana Gladys Wanga.

Viongozi hao, kwa kauli moja wakitoa wito kwa wakazi kuunga mkono serikali jumuishi ili kunufaika na miradi mingi zaidi ya maendeleo siku zijazo.

Ni wakati huo ambapo Rais Ruto kwa mara nyingine aliushambulia upinzani aliyosema hauna ajenda, maono wala mipango ya kuifaidi nchi mbali na kaulimbiu za wantam na Kasongo. 

 

Share This Article