Kenzo ajitenga na wanablogu wanaomdai Bebe Cool

Anasema kuhusishwa kwake na sakata hilo ni njia ya kuvuruga mjadala na kuondoa umakini kutoka kwa vijana hao wa mitandao ya kijamii wanaodai kulipwa.

Marion Bosire
2 Min Read
Eddy Kenzo

Mwanamuziki wa Uganda Eddy Kenzo amejibu madai yanayomhusisha na kundi la washawishi wa tandao wa TikTok wanaodai malipo kutoka kwa Bebe Cool kwa kazi wanayodai kufanya wakati wa kampeni za NRM.

Kenzo amepuuza madai hayo akiyataja kuwa “upuuzi” akisema jina lake linatajwa katika mzozo huo kutokana na ushawishi wake pamoja na ushindani wa muda mrefu kati yake na Bebe Cool.

Kulingana na Kenzo, kumhusisha na sakata hilo ni njia ya kuvuruga mjadala na kuondoa umakini kutoka kwa vijana hao wa mitandao ya kijamii wanaodai kulipwa.

Kenzo alijieleza kwa ujasiri kuwa yeye ndiye humtishia zaidi Bebe Cool, akidai umaarufu na ushawishi wake humfanya kuwa mlengwa rahisi kila kunapotokea utata unaohusisha kambi ya Gagamel anayomiliki Bebe Cool.

Msanii huyo pia alisisitiza kuwa hana nia ya kuhusika katika mzozo huo na kwa sasa anaangazia muziki wake.

Kenzo alikiri kuwa yeye na Bebe Cool waliwahi kutofautiana wakati wa kampeni za NRM, hasa kuhusu namna vyombo vya habari vilikuwa vikirekodi maonyesho yao.

Hata hivyo, alisema suala hilo lilitatuliwa wakati huo na halipaswi kuhusishwa na madai ya sasa ya wanamitandao kuhusu malipo.

Kenzo alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana Bebe Cool ashughulikie masuala ya vyombo vya habari na wasanii wa kitaifa, huku yeye akisimamia wasanii wa kikanda.

Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya kudaiwa kuambiwa vyombo vya habari visirekodi maonyesho yake ya kampeni.Alisema baadaye alijipangia huduma yake ya vyombo vya habari na kuendelea na maisha bila kuendeleza mzozo huo.

Share This Article