Maafisa wawili wa mahakama wakamatwa kwa madai ya ufisadi

Wawili hao walikamatwa baada ya EACC kutekeleza operesheni tofauti mjini Nakuru na Eloret.

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wawili wa mahakama wakamatwa kwa madai ya ufisadi.

Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imewakamatwa maafisa wawili wa mahakama, kwa madai ya kuitisha na kupokea hongo ili kutoa huduma za mahakama.

Wawili hao walikamatwa baada ya EACC kutekeleza misako tofauti mjini Nakuru na Eloret.

Mjini Eldoret, maafisa wa EACC  walimkamata msaidizi wa mahakama  Linet Okungu kwa kuitisha na kupokea hongo ya shilingi 20,000 mnamo tarehe 8 Septemba, 2026.

Kulingana na maafisa wa EACC, fedha hizo zilikuwa sehemu ya hongo ambayo afisa huyo alikuwa ameitisha ili asaidie kutoa agizo la mahakama kuzuia uuzaji wa ardhi kwenye kesi iliyo mahakamani.

Mshukiwa huyo ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi 20,000, huku uchunguzi ukiendelea.

Katika kisa tofauti kaunti ya Nakuru, maafisa wa EACC walimkamata Bernard Ngeno ambaye ni afisa wa usajili kwa kupokea hongo ili atenge tarehe mwafaka ya kusikilizwa kwa kesi ya mlalamishi.

Ngeno aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 5,000 akisubiri kukamilishwa kwa uchunguzi.

“Kukamatwa kwa wawili hao ni ishara ya kujitolea kwa tume hii kukabiliana na rushwa na aina zingine za ufisadi na kuimarisha utoaji huduma bora kwa wananchi wote,” ilisema EACC kwenye taarifa.

Share This Article