Watu zaidi ya 300 wamefariki kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku taifa hilo likijizatiti kujinasua kutoka kwa chamko la ugonjwa huo hatari.
Taarifa ya Wizara ya Mawasiliano na Vyombo vya Habari nchini DRC, imesema jumla ya watu 1,155 wamethibitishwa kuambukizwa Ebola, wagonjwa 304 wamefariki kutokana na makali ya ugonjwa huo, na wengine 326 wametengwa au wanapokea matibabu.
DRC imechukua hatua kali za kudhibiti msambao wa ugonjwa huo, hususan kwa wale wanaosafiri kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Ebola.
Chini ya sheria iliyotiwa saini na Waziri wa Afya Roger Kamba siku ya Jumatano, maafisa wa afya, wale wa maabara na wale wa makundi ya dharura wanaorejea kutoka maeneo yanayoathiriwa na Ebola, ni sharti wajitenge kwa siku 21, huku wakizuiwa kusafiri ndani au nje ya nchi wakati wa kipindi hicho.
Chamko la ugonjwa huo lililotangazwa katikati ya mwezi Mei mwaka huu, limesababishwa na aina ya Bundibugyo ambayo hadi sasa haina tiba.