Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi nchini Venezuela siku ya Jumatano imeongezeka hadi watu 188 huku wengine 1,520 wakijeruhiwa.
Hayo yametangazwa na Rais wa Bunge la Taifa Jorge Rodriguez siku ya Alhamisi.
Akizungumza kwenye runinga ya taifa, Rodriguez alisema nchi hiyo inajaribu iwezavyo kuwaokoa majeruhi walionaswa kwenye vifusi, akidokeza kuwa idadi ya waathirawa wa mkasa huo itaendelea kutangazwa.
Watu zaidi ya 200 walikuwa wamenaswa kwenye vifusi na 157 hawakujulikana walipo.
Kulingana na Rodriguez, serikali ya Venezuela imetangaza baadhi ya sehemu za taifa hilo kuwa maeneo ya mkasa, ikiwa ni pamoja na eneo La Guaira.
Takriban nyumba 346 ziliharibiwa na tetemeko hilo, ikiwa ni pamoja na hospitali 8 huku wakazi wakihamishwa.
Rodriguez alisema makundi ya kimataifa ya uokoaji kutoka mataifa kadhaa tayari yamewasili nchini Venezuela kusaidia katika utoaji misaada.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutoa misaada ya bidhaa msingi na kuziwasilisha kwa maeneo husika kote nchini humo.
Maafisa wa uokoaji wangali wanawatafuta manusura kwenye majengo yaliyoporomoka, huku magari ya uokoaji pia yakiwasili.
Kutokana na hofu, raia wengi wa Venezuela walianza kulala barabarani au ndani ya magari.