Watu 355 wamekamatwa kote nchini Kenya kwenye maandamano yaliyoandaliwa kuwakumbuka vijana wa Gen-Z waliofariki mwaka 2024.
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen kwenye mkutano na wanahabari Jijini Nairobi, alisema baadhi ya watu walijaribu kuvuruga maandamano ya amani, na kusababisha maafisa wa polisi kuingilia kati na kuwakamata.
Kulingana na Murkomen, Kaunti ya Nairobi ikiongoza kwa idadi ya waliokamatwa ambapo washukiwa 161 walikamatwa, kaunti ya Kajiado ikuafuata huku washukiwa 123 walikamatwa, Kiambu (36), Murang’a (12), Bungoma (9), Meru (6), Laikipia (5), na Machakos (3).
Murkomen, aliwapongeza maafisa wa usalama kwa kuhakikisha usalama unadumishwa wakati wa maandamano hayo.
“Nawapongeza maafisa wa usalama kwa kujitolea kwao kudumisha amani. Walitekeleza majukumu yao kwa utaalam wa hali ya juu na kushughulikia wasiwasi ulioibuliwa na Wakenya,” alisema Murkomen.
Aidha, alithibitisha kuwa Naibu wa Chifu wa kata ndogo ya Kariti, kaunti ya Murang’a Anthony Kathungu, alijeruhiwa kwenye maandmanao hayo, baada ya kushambuliwa na kundi la watu lililotaka kufunga barabara katika eneo la Kandara.
“Alitibiwa na yuko katika hali dhabiti,” alisema Murkomen.