Serikali yatakiwa kuagiza mahindi meupe kukabili uhaba

Kenya inakabiliwa na uhaba wa mahindi kutokana na uzalishaji mdogo wa zao hilo msimu huu, hususan kutokana na ukame ulioshuhudiwa nchini, miongoni mwa mambo mengine.

Martin Mwanje
2 Min Read
Picha kwa hisani ya KNA

Serikali inatafakari ombi la viwanda vya kusaga mahindi la kuagiza tani metriki milioni 3 za mahindi meupe yasiyotozwa ushuru ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

Viwanda hivyo vinasema hatua hiyo itasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya kupanda kwa bei za unga kutokana na uzalishaji mdogo wa mahindi msimu huu.

Vilitoa ombi hilo kupitia Chama cha Viwanda vya Kusaga Mahindi nchini, CMA wakati wa mkutano kati ya maafisa wake wakiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Paloma Fernandes na Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe.

Katika kutoa ombi hilo, Fernandes alisema Kenya inakabiliwa na uzalishaji mdogo zaidi wa mahindi kuwahi kutokea huku kaunti sita pekee zinazozalisha zao hilo zikitarajiwa kuwasilisha magunia milioni moja msimu huu.

“Huu ndio uzalishaji mdogo zaidi na ni suala kubwa kwetu,” alisema Fernandes wakati wa mkutano ulioitishwa na Kagwe ukiwaleta pamoja wadau katika sekta hiyo.

CMA inataka kipindi cha uagizaji wa mahindi hayo kuwa miezi 9 ili kuwapa waagizaji muda wa kutosha kuandikisha mikataba, kufadhili na kufanya mipango ya usafirishaji wa bidhaa hiyo.

Ni ombi ambalo lilionekana kuungwa mkono na Waziri Kagwe aliyesema serikali lazima ichukue hatua za mapema za kuhakikisha kuna mahindi ya kutosha nchini.

“Hatuwezi kumudu kutokuwa na mahindi,” alisema Kagwe.

Zambia na Tanzania zimeibuka kuwa nchi ambazo mahindi hayo yanaweza kuagizwa huku Balozi wa Kenya nchini Zambia Lilian Tomitom akithibitisha kuwepo kwa bidhaa hiyo nchini humo.

Waziri Kagwe ametoa wito wa mazungumzo kufanywa na serikali ya Zambia kupunguza bei ya kununua na kusafirisha mahindi hayo.

Na ingawa ombi la uagizaji mahindi meupe linazingatiwa, Waziri aliashiria kuwa serikali inadhamiria kuchapisha kwenye gazeti rasmi utengenezaji wa tani metriki 360,000 za mahindi ya njano ya kutumiwa kama malisho ya mifugo.

Hata hivyo, Kagwe alionya kuwa ongezeko la uagizaji wa mahindi haupaswi kuhatarisha usalama wa chakula, akisisitiza kuwa mahindi yote yanayoingia nchini yanapaswa kukidhi viwango vilivyowekwa ikiwa ni pamoja na usafi, unyevunyevu na masuala ya sumu ya aflatoxin.

“Msilete mahindi ambayo hayatakidhi viwango. Hakupaswi kuwa na mahindi katika ghala zetu ambayo yameharibika,” alionya Kagwe.

Share This Article