Rais wa Gambia Adama Barrow amesema taifa hilo litaimarisha usambazaji wa umeme kufikia mwezi ujao, huku maanadmano yakishuhudiwa kote nchini humo kutokana na ukosefu wa umeme kwa muda mrefu.
Waandamanaji ambao waliteketeza magurudumu na kufunga barabara katika mji mkuu wa nchi hiyo, Banjul juzi Jumatatu na Jumanne, wanashinikiza kujiuzulu kwa Rais Barrow.
Maafisa wa polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya waandamanji ambao pia walikuwa wamekusanyika karibu na makao ya Rais Barrow na katika Makao Makuu ya Shirika la Maji na Umeme (NAWEC), ambalo husambaza umeme kote nchini humo.
Kwenye hotuba yake kwa taifa, Rais Barrow alitangaza kuwa serikali itajenga kiwanda cha umeme kinachotumia miale ya jua cha megawati 24 kufikia mwisho wa mwezi Oktoba.
Ukosefu wa umeme katika taifa hilo la Afrika Magharibi umejiri wakati wa msimu wa joto na umedumu hadi saa 48 katika baadhi ya maeneo.