Rais Ruto apongeza ufanisi wa kongamano la Africa Forward

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwenye hafla ya kufunga kongamano la Africa Forward kwenye uwanja wa Kasarani.

Rais wa Kenya William Ruto amepongeza ufanisi wa kongamano la 4 la Africa Forward lililoandaliwa Jijini Nairobi, akisema ufanisi huo ni thibitisho la utamaduni wa Afrika, talanta na ubunifu.

Kongamano hilo liliandaliwa Mei 11 na 12, Jijini Nairobi na liliwaleta pamoja Marais 30 wa bara Afrika na wajumbe 4,000 kutoka pembe zote za dunia.

Akizungumza kwenye warsha ya kufunga rasmi kongamano hilo katika ukumbi wa uwanja wa michezo wa Kaasarani Jumanne jioni, Ruto alisema mitindo, miziki na densi zilizosheni hafla hiyo zilidhihirisha uwezo na utofauti wa bara la Afrika na pia kubaini uwezo wa vijana wa bara hili kwenye ubunifu.

“Maonyesho hayo yalikuwa yakupendeza na yalidhihirisha utamaduni wa Afrika, talanta, ubunifu na uvumbuzi wa vijana wetu,” alisema Rais Ruto.

Maonyesho ya densi na nyimbo, kwenye hafla ya kufunga kongamano la Africa Forward, Kasarani, Nairobi.

Kiongozi wa taifa aliwapongeza washirika wote husika, wadhamini na waliohudhuria kwa kuunga mkono kongamano hilo lililowaleta pamoja viongozi na wajumbe kutoka kote ulimwenguni.

“Kwa niaba ya serikali na watu wa Kenya nawashukuru washiriki wote, wafadhili na wadau waliochangia katika ufanisi wa kongamano hili la kihistoria,” aliongeza Rais Ruto.

Wakati huo huo, Rais Ruto alimshukuru Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kwa kupiga jeki juhudi zinazolenga kuboresha ushirikiano baina ya bara Afrika na Ufaransa.

Share This Article