Bien ateuliwa kuwania tuzo ya Headies

Anashindana na Watanzania Abigail Chams na Harmonize, Bruce Melodie wa Rwanda na Joshua Baraka kutoka Uganda

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Bien-Aimé Baraza, ameteuliwa kuwania tuzo katika awamu ya 18 ya tuzo za Headies na hivyo kuiweka Kenya katika nafasi nzuri kimataifa.

Baraza ambaye awali alikuwa akiimba kwenye kundi la Sauti Sol lililosambaratika, atakuwa anawania tuzo katika kitengo cha Msanii Bora wa Mwaka kutoka Afrika Mashariki.

Atakuwa anapambana na Watanzania Abigail Chams na Harmonize, Bruce Melodie wa Rwanda na Joshua Baraka kutoka Uganda, huku hafla ya kugawa tuzo hizo ikipangwa kuandaliwa Oktoba 23 hadi 25, 2026 jijini Toronto nchini Canada.

Awamu hii ya 18 ya tuzo za Headies ina vitengo takribani 35, vinavyojumuisha msanii bora mpya wa mwaka, Msanii bora wa mtindo wa Street-Hop, wimbo bora wa mwaka na albamu bora ya mwaka.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Africa to the World” ambapo muziki wa Nigeria na Afrika utatambuliwa.

Chimbuko la tuzo za Headies ni nchini Nigeria na zilianzishwa na Ayo Animashaun mwaka 2006, wakati huo akizirejelea kama Hip Hop World Awards.

Baadaye jina hilo lilibadilishwa na kuwa The Headies mwaka 2011 na kutoka jijini Lagos, nchini Nigeria zilikapanuka na kuwatambua wasanii kutoka maeneo mengine ya Afrika pamoja na wasanii wa Afrobeats kutoka duniani kote.

Sauti Sol waliteuliwa kuwania tuzo ya Headies mwaka 2016 na sasa ni zamu ya Bien kama msanii huru.

Share This Article