Phiona Nyamutoro aelekeza video ya mumewe

Alichapisha picha zinazomwonyesha akihusika katika maandalizi ya video ya wimbo "Nkulowoza" wa Eddy Kenzo.

Marion Bosire
1 Min Read

Phiona Nyamutoro ambaye ni waziri wa madini nchini Uganda, kwa muda alijivua ukuu wake kama waziri serikalini na kuamua kuhusika katika maandalizi ya video ya muziki ya mume wake.

Wikendi hii ya Pasaka, waziri huyo wa umri wa miaka 31, ambaye ni mke wa mwanamuziki Eddy Kenzo, alijiunga na kundi la maandalizi ya video ya wimbo wa Kenzo uitwao “Nkulowoza”.

Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii jana Jumamosi, Nyamutoro aligusia jukumu lake jipya akisema, “Mtu angenionya kwamba siku moja nitakuwa mwelekezi asiyelipwa wa video.”

Alimtania pia meneja wa Eddy Kenzo huku akimwonya kwamba hivi karibuni huduma zake zitakuwa za kitaalamu na hivyo anastahili kumweka kwenye orodha ya wanaolipwa wakati huu ambapo anaweza kummudu.

Waziri huyo vle vile alihimiza wapenzi wa muziki wa Kenzo kutazama video hiyo kwenye mtandao wa YouTube wanaposherehekea pasaka.

Nyamutoro na Kenzo walifanya sherehe ya kitamaduni ya uchumba Juni 29, 2024 na kufikia sasa wamebarikiwa na mtoto wa kiume.

Kando na muziki, Kenzo ambaye jina lake halisi ni Edrisah Musuuza, anahudumu kama mshauri mkuu wa Rais Yoweri Museveni kuhusu wabunifu nchini Uganda.

Website |  + posts
Share This Article