Jamii zinazoshi kando ya fukwe za bahari huko Kwale katika maeneo kama Tsunza, Waa, Tiwi, Mwaepe, Msambweni, Mkwiro na Vanga kwa muda mrefu zimekuwa zikitegemea uvuvi kama chanzo kikuu cha riziki.
Hata hivyo, ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uvuvi, mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa ujuzi wa kutosha wa uvuvi vimesababisha kiwango kidogo cha samaki wanaovuliwa.
Hali hiyo inasababiisha kiwango cha mapato kupungua na hivyo kutishia uwezo wao wa kukidhi mahitaji ya msingi.
Jamii hizi sasa zimepata afueni baada ya kupokea msaada kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Kwale kupitia mradi wa Kenya Marine Fisheries and Socio-Economic Development (KEMSFED) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Kupitia mradi huu, Kaunti ya Kwale ilisambaza boti 59 za kisasa za uvuvi, vifaa vya kutambua samaki (fish finders), vifaa vya GPS, pamoja na mashine za kuongeza thamani ya samaki miongoni mwa vifaa vingine vya uvuvi.
Vifaa hivyo vimeongeza kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka kilo 2 au 3 kwa siku hadi zaidi ya tani 1.5 kwa siku.
Gavana wa Kwale Fatuma Achani amesema kuimarishwa kwa sekta ya uvuvi ni njia moja ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya jamii za wavuvi kaunti hiyo.
“Mpango huu si wa kuongeza tu kiasi cha samaki wanaovuliwa, bali ni wa kuboresha maisha ya wavuvi na familia zao. Ni hatua kuelekea katika ustawi wa muda mrefu kwa watu wa Kwale” alisema Gavana Achani.
Kwa mujibu wa waziri wa kaunti ya Kwale wa masuala ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Roman Shera, mradi wa KEMSFED pia umechangia ujenzi wa vituo 9 vya kupokelea samaki (landing sites) vilivyo na vifaa vya kuhifadhi samaki kwenye baridi pamoja na vifaa vya kisasa vya kuendeleza sekta hiyo.
Vituo hivyo vidogo vya bandari ni pamoja na Shimoni, Vanga, Gasi, Chale, Tsunza katika Kaunti Ndogo ya Kinango na maeneo mengine.
“Vituo hivi vinaruhusu wavuvi wetu kuhifadhi samaki kwa muda mrefu, kupunguza hasara na kuongeza faida yao” alisema Shera.
Kupitia mradi huo, wavuvi 76 wamefunzwa kuwa waendeshaji boti wakiwemo wanawake 4 na wamepatiwa ujuzi wa kuwawezesha kufanya uvuvi katika bahari kuu.
“Mafunzo haya yametufundisha mbinu bora zaidi za uvuvi na tunafurahi kuwa ubora wa samaki tunaovua umeimarika” alisema Halima Hamisi, mmoja wa marubani waliofunzwa.
Kwa upande wake, Mohammed Mbogo, mvuvi wa eneo la Tsunza, alieleza shukrani zake kwa serikali ya kaunti, akiongeza kuwa ujio wa vifaa vya kisasa vya uvuvi umebadilisha maisha yao.
“Hapo awali tulikuwa tunategemea vifaa vya jadi na wengi wetu tulikuwa tukishindwa hata kupata samaki wa kutosha kwa familia zetu. Sasa, kwa boti hizi mpya, tunaweza kufika maeneo ya ndani zaidi ya bahari na kuvua samaki kwa wingi. Ni mwanzo mpya kwetu” alisema Mbogo.
Mafanikio ya mradi wa KEMSFED yameleta matumaini mapya kwa jamii za wavuvi wa Kwale, kwa kuwapatia nyenzo na ujuzi wa kuweza kustawi katika soko la ushindani.
Kwa msaada endelevu kutoka kwa serikali ya kaunti na wadau wa kimataifa kama Benki ya Dunia, wavuvi wa Kwale sasa wanatazamia maisha yenye mwangaza zaidi.