Mwigizaji wa kike Nigeria Iyabo Ojo amemiminiwa sifa nyingi mitandaoni kwa kile kinachosemekana kuwa hatua yake ya kudhihirisha ukomavu katika harusi ya binti yake Priscilia.
Hii ni baada ya mama huyo wa watoto wawili kukubalia baba mzazi wa binti yake kwa jina Ademidun Ojo, kuhusika katika ndoa yake.
Awali wakati wa awamu ya Tanzania ya ndoa ya Priscilia na Juma Jux, babake hakuwepo suala lililozua minong’ono mitandaoni wengi wakidhania kwamba alifungiwa nje.
Dhana hiyo inatokana na ukweli kwamba Iyabo Ojo amekuwa akilea wanawe peke yake kwa muda mrefu baada yake na baba yao kutalikiana.
Wanandoa hao wa zamani waliweka kando tofauti zao na kuungana kwa ajili ya tukio kubwa katika maisha ya binti yao ambaye alifanya harusi ya kitamaduni kulingana na tamaduni za kabila la Yoruba.
Jana Priscilla na Jux walifanya harusi ya kanisa hata ingawa Jux ni muumini wa dini ya kiisilamu na Priscilla ni mkiristo.
Ademidun na Iyabo waliketi pamoja wakati wa kutoa mwanao kwa ajili ya ndoa na walikuwa wamevaa mavazi ya kufanana.
Iyabo aliolewa na Ojo, mwaka 1999 akiwa na umri wa miaka 21 hatua iliyomfanya aache kazi ya uigizaji kwa muda.
Mwaka 1999 alibarikiwa na mwanao wa kwanza wa kiume kwa jina Felix huku Priscilia akizaliwa mwaka 2001 na mwaka huo huo ndio walitalikiana.
Kulingana na Iyabo, ndoa yake ilivunjika kwa sababu aliolewa akiwa na umri mdogo. Sasa yuko kwenye uhusiano wa kimapenzi na jamaa kwa jina Paulo ambaye pia alihudhuria harusi ya Priscilia lakini hakuwa mstari wa mbele labda katika hatua ya kuwapa wazazi halisi nafasi ya kusherehekea ndoa ya mwanao.
Ademidun Ojo ambaye sasa anaishi nchini Marekani naye anaripotiwa kuwa na mke na wana mtoto wa kiume.