Wanachama wa Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Nishati, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, ambaye ni Seneta wa kaunti ya Elgeyo Marakwet William Kisang, walimtembelea na kumpa pole Seneta wa Kakamega Boni Khalwale.
Walimtembelea katika makazi yake ya Malinya, Kakamega kumfariji kufuatia kifo cha mkewe, Gloria Sekeiyan Khalwale.
Akitamka maneno ya kumtia moyo Seneta Khalwale, ambaye ni mwanachama wa Kamati hiyo, Seneta Kisang alimtaka amshukuru Mungu kwa miaka aliyoshirikiana na marehemu mke wake pamoja na baraka ambazo Mungu aliwajalia.
“Kama Kamati, tumeleta salamu zetu za pole za dhati kwako wewe pamoja na familia yako. Mshukuru tu Mungu kwa miaka aliyokupa pamoja naye na kwa baraka alizokujalia. Hakuna jambo unaloweza kufanya kuhusu hilo sasa,” alisema.
Seneta mteule Beatrice Ogolla, ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema kifo cha ghafla cha Gloria kimeshtua taifa akimtaka Khalwale akubali mapenzi ya Mungu, huku akisisitiza kuwa Kamati iko kikamilifu nyuma ya Seneta wa Kakamega.
Seneta wa Turkana James Lomenen alimtia moyo mwenzake kumwomba Mungu kila mara amwiminie neema Yake tele, huku akiwasilisha salamu za pole kutoka kwa wananchi wa Turkana.