Nandor aibuka na aina tofauti ya tamasha

Amewataka mashabiki wajiandae kuvaa kama wanyama; twiga, pundamilia, chui, simba na wengineo siku hiyo.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Nandor Love ameibuka na mtindo tofauti wa tamasha huko akionjesha onjesha mashabiki zake wanayotarajia kwenye tamasha yake ijayo.

Akizungumza katika mahojiano, mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Nantume Dorcus Tendo, alisema kwamba hafla hiyo ijayo itajikita sana katika masuala ya wanyama ambao huwa anawaimba mara nyingi.

“Hivi karibuni nitaandaa tamasha yangu. Jiandaeni kuvaa kama wanyama; twiga, pundamilia, chui, simba na wengineo, kwa sababu hicho ndicho ninachoimba vizuri zaidi,” alisema mrembo huyo.

Mwimbaji huyo alisema atatangaza rasmi maelezo zaidi ya tamasha hiyo hivi karibuni, na kuwaacha mashabiki wakijiandaa kwa usiku wa kipekee wenye mandhari maalum, utakaoadhimisha muziki wake pamoja na upendo wake kwa wanyamapori.

Nandor Love ambaye sasa ana umri wa miaka 23, ana nyimbo kadhaa, wimbo wake wa kwanza “Baby Boo” ukiwekwa kwenye akaunti yake ya YouTube miaka minne iliyopita.

Ameimba nyimbo kama Mpologoma neno linalomaanisha Simba, Embuzi linalomaanisha mbuzi na Embalasi linalomaanisha farasi kwa lugha yake.

Hata ingawa nyimbo hizo zina majina ya wanyama, mwimbaji huyo ameziendeleza kwa maudhui ya mapenzi na hata yale ya jamii kwa jumla.

Share This Article