Jukwaa la kusambaza video na muziki mitandaoni la Spotify limepiga hatua katika kukabiliana na ongezeko la muziki unaozalishwa kwa kutumia akili unde yaani AI.
Usimamizi wa jukwaa hilo umeanza kuweka utambuzi wa “AI Persona” kwenye wasifu wa baadhi ya Wasanii wanaoundwa na teknolojia hiyo.
Alama hiyo inadhamiriwa kuwasaidia wanaotumia jukwaa la Spotify kutambua kwa urahisi ikiwa wanamsikiliza Msanii halisi au kazi za muziki zilizoundwa kwa kutumia AI.
Haya yanajiri huku akili mnemba ikiendelea kusababisha mabadiliko makubwa katika tasnia ya muziki, kuanzia utengenezaji wa nyimbo na sauti hadi namna kazi za wasanii zinasambazwa na kuishia kwao kupata umaarufu.
Wapenzi wa muziki wanaweza kupata hatua hii ni muhimu zaidi kwao kadri Wasanii wa Akili Unde wanavyozidi kuonekana kwenye majukwaa ya muziki mtandaoni.
Spotify pia inaonekana kutaka kuongeza uwazi kwa wasikilizaji, ili mtu anapokutana na msanii au mradi wa muziki uliotengenezwa na AI, aweze kujua hilo mapema badala ya kudhani kuwa ni Msanii halisi.