Chameleone amshukuru Mungu kwa nafuu

Chameleone alilazwa hospitalini nchini Marekani siku chache zilizopita kwa ajili ya upasuaji.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Jose Chameleone ameashiria kwamba anaendelea kupata nafuu na kwamba upasuaji aliofanyiwa wa kongosho ulifanikiwa.

Alifanya hivyo kwa kuchapisha picha akiwa bado kwenye chumba cha hospitali na kuandika, “Asante Mungu. Nitaendelea kukushukuru milele. Jina lako litukuzwe baba.”

Msanii huyo alichapisha video awali ya kufahamisha wanaompenda kwamba alikuwa anajiandaa kwa ajili ya upasuaji huo na kuahidi kuendelea kuwapa habari kuhusu hali yake.

Katika video hiyo ya awali vile vile alilalamikia uchapishaji wa habari potovu kumhusu kwenye mitandao ya kijamii akisema hatua kama hiyo ina madhara.

Kufikia sasa muhusika wa utoaji wa habari hizo za uongo ambaye ni mtangazaji wa redio Janie Namukasa ameomba msamaha na kutubu kwa kuhadaa umma kwamba Jose alikuwa ametiwa mbaroni nchini Marekani.

Chameleone amekuwa nchini Marekani tangu Disemba 2024 alikopelekwa na kakake Douglas Mayanja au ukipenda Weasel Manizo na rafiki yake Juliet Zawedde ambaye pia ni mwenyeji wao nchini Marekani.

Msanii huyo nguli anatumai atarejelea hali ya kawaida baada ya kupona ugonjwa wa kongosho unaodaiwa kusababishwa na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Website |  + posts
Share This Article