Nyota Ndogo afafanua kuhusu umri wake

Aliwaondolea wasiwasi mashabiki waliompa umri mkubwa kuliko alionao, akisema anajivunia umri wake wa miaka 45.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Nyota Ndogo alilazimika kufafanua kuhusu umri wake, baada ya kubanwa na shabiki mtandaoni, akisema hana sababu ya kuuficha na kwamba kwa sasa ana miaka 45.

Kupitia ujumbe wake, Nyota Ndogo aliwaondolea wasiwasi mashabiki waliokuwa wakimpa umri mkubwa kuliko alionao, huku akisema anajivunia umri wake.

“Nina umri wa miaka 45 na ninajivunia,” alisema, akitania kwamba watu wanaweza hata kuongeza miaka ya wazazi wao kwake, kwa kuwa hana tatizo na hilo.

Msanii huyo pia alizungumzia madai kwamba ana miaka 60 kwa sababu alianza kuimba wakati baadhi ya mashabiki walikuwa bado wanafunzi wa darasa la nane.

Alieleza kuwa tofauti ya maisha ndiyo iliyofanya aonekane mkubwa zaidi kiumri.

Kwa mujibu wa Nyota Ndogo, wakati baadhi ya watu waliendelea na masomo, yeye alilazimika kuacha shule na kuanza kutafuta pesa mapema kupitia muziki.

Alisema changamoto za maisha zilimlazimisha kukua haraka, lakini hilo halimaanishi kwamba ana miaka 60.

Nyota Ndogo alisisitiza kuwa siku atakapofikisha miaka 60, atasherehekea kwa mbwembwe, akiamini kuwa Mungu atakuwa amemwongezea miaka mingine mitano.

Aidha, alitania kuwa huenda akawapa mashabiki amani ya moyo kwa kukubali tu kwamba ana miaka 60.

Share This Article