Prezzo asimulia alivyokataliwa na P-Funk

Alikwenda kwa Micah Mwamba ambaye pia ni mtayarishaji muziki, ambapo walitengeneza wimbo “Let’s Get Down” akiwa na Nazizi.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Kenya CMB Prezzo amekuwa kwenye ziara nchini Tanzania ambapo aliungana na wasanii wakongwe wa muziki kuadhimisha miaka 30 ya Bongo Fleva.

Akiwa nchini humo, alihojiwa na wanahabari ambapo alisimulia kuhusu safari yake ya muziki nchini Tanzania.

Prezzo ambaye jina lake halisi ni Jackson Ngechu Makini, alielezea jinsi mtayarishaji maarufu wa muziki nchini Tanzania P-Funk Majani aliwahi kukataa kufanya kazi na yeye.

Prezzo alisema wakati huo alitoka Kenya akiwa na matarajio ya kufanya kazi na Bongo Records yake P-Funk Majani, akiamini kuwa  angekuwa sehemu muhimu ya safari yake ya muziki.

Hata hivyo, alisema P-Funk alikataa kufanya naye kazi, licha ya mama yake mzazi kumlipia gharama za muda wa kutumia studio.

Baada ya kukataliwa, alikwenda kwa Micah Mwamba ambaye pia ni mtayarishaji muziki, ambapo walitengeneza wimbo “Let’s Get Down” akiwa na Nazizi. Wimbo huo ulifanya vizuri .

Msanii huyo anasema kwamba mpaka sasa hajafahamu sababu iliyomfanya P-Funk amkatae, lakini anaamini huenda Mungu alikuwa na mpango mwingine kwake, kwani kukataliwa  ndiko kulimfungulia njia ya mafanikio.

Alipokwenda kutumbuiza kwenye awamu ya Mwanza ya tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva, Prezzo alifichua kwamba mamake mzazi ni mzaliwa wa Mwanza na alikuwa akijihisi nyumbani.

Share This Article