Profesa Jay apokea msaada kutoka kwa Rais Samia

Alipokea shilingi milioni 30, pesa za Tanzania, kutoka kwa Rais wa Samia kumwezesha kuendelea na maisha baada ya kuugua.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki tajika wa mtindo wa Hip Hop nchini Tanzania Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, amepokea msaada wa kifedha kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Nyota huyo aliyewahi kuhudumu kama mbunge wa Mikiumi, alipokea shilingi milioni 30, pesa za Tanzania, kutoka kwa Rais wa Samia kumwezesha kuendelea na maisha yake baada ya kutoka kwenye changamoto ya afya iliyokuwa ikimkabili.

Alikabidhiwa fedha hizo jana mei 10 2026 na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ambaye pia ni mwanamuziki, aliyemtembelea Prof Jay.

Mheshimiwa Mwinjuma alikuwa ameandamana na Mstahiki Meya wa jiji la Dar es salaam Nurdin Bilal Juma almaarufu Shetta.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulimfikishia Prof Jay salamu maalum kutoka kwa Rais Samia, huku ukieleza kuwa Serikali inaendelea kuthamini mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki na jamii kwa ujumla.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Prof Jay alimshukuru Rais Samia kwa moyo wake wa upendo na namna alivyoendelea kumuunga mkono tangu alipokuwa akisumbuliwa na maradhi hadi aliporejea katika hali yake aidha amewashukuru Watanzania waliokuwa wakimuombea na kumpa faraja katika kipindi chote cha changamoto alizopitia.

Mei Mosi, wakongwe wa muziki wa Bongo walimwandalia tamasha Profesa Jay ambapo pia alipokea tuzo ya Bongo Fleva Honors, huku akionjesha mashabiki kazi zake.

Share This Article