Mwigizaji Patrick Serro ambaye wengi wanamfahamu kwa jukumu lake katika kipindi cha Makutano Junction alikoigiza kama Dkt. Washington amefariki.
Ripoti zinaashiria kwamba Serro alikata roho Januari 25, 2025 muda mfupi baada ya kulalamikia maumivu ya kifua akiwa nyumbani.
Taarifa za kifo chake zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii na dadake kwa jina Ascar Serro Ogombe, aliyeelezea kwamba siku hiyo, Patrick alikuwa ametoka gereji na alikuwa akitazama video za kazi zake za awali alipopata maumivu.
Ascar alimwomboleza kakake akisema amekuwa nguzo muhimu kwa maisha yao baada ya wazazi wao kuaga dunia zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Aliendelea kuelezea kwamba Patrick alimtumia ujumbe kumjuza kwamba hajihisi vizuri na alikuwa anaelekea hospitali na alipomfuata huko akafahamishwa kwamba ameshafariki.
“Nenda salama kakangu Patrick Serro. Hadi tutakapokutana tena,” alimalizia Ascar.
Binti ya Patrick ambaye ni mwanamuziki anayefahamika kwa jina Serro naye alimwomboleza babake akikiri kwamba alimpenda hadi alipovuta pumzi ya mwisho.
Alichapisha video ya babake akicheza densi na kuandika, “Nimevunjika moyo baba! Nilipoandika wimbo huu sikujua nitauimba kukuomboleza lakini yameshafanyika.”
Serro aliahidi kujitahidi kumfurahisha babake na kubeba jina la familia kwa majivuno.
“Naskia huko juu muziki inabamba sana. Nitakubeba moyoni kila mara. Pumzika baba,” alimalizia.
Carolyne Midimo ambaye aliwahi kuigiza pamoja na Patrick naye aimwomboleza kupitia mitandao ya kijamii ambapo alichapisha video yake akicheza densi.
Alielezea kwamba ilikuwa wakati wa sherehe yao ya kufunga mwaka mwezi Disemba mwaka 2024 ambapo kulingana naye alikuwa mwenye nguvu na furaha.
Midimo alisema pia kwamba aliwasiliana naye Jumamosi saa chache kabla ya kufariki huku akimlaumu kwa kutomjuza kwamba anaenda.
“Ni nini kilifanyikia heshima ya urafiki wetu? Mimi sijui hata nianze vipi kukuomboleza, Umenivunja. Umetumaliza. Hiyo Studio haitakuwa sawa tena. Nitakubeba moyoni kila mara. Pumzika,” ndiyo baadhi ya maneno aliyoandika Midimo.
Waigizaji wenza pamoja na mashabiki pia wamemwomboleza Patrick Serro kwenye mitandao ya kijamii huku wakikumbuka kazi zake.